Usithubutu ‘kufeki’, penzi bora hujitengeneza lenyewe -2
Bila shaka wasomaji wangu wote ni wazima wa afya na mnaendelea na majukumu yenu. Tunaendelea na mada yetu kuanzia pale tulipoishia.
Twende pamoja...
MZEE Nelson Mandela ‘Madiba’, alitoa talaka kwa bibi yetu, Winnie. Waliishi miaka mingi, wakazaa watoto ambao wengine kwa sasa ni wakubwa kabisa. Baadaye akagundua Winnie si bahati yake, leo yupo kwenye ndoa na Graca Machel, maisha yanaendelea.
Kumbe Graca ndiye bahati ya Mzee Mandela. Ilivyo ni kwamba Winnie alitangulia kwa lengo la kukamilisha safari ya maisha ya babu yetu huyo anayeheshimiwa mno duniani. Chukua mfano huo, halafu jipe matumaini. Maisha ni matamu mno bila ya huyo wako ambaye si bahati yako.
Napenda tena nitie mkazo kwamba mapenzi ni magumu. Kama Mandela yalimuumiza, inashindikana vipi kwako? Ukimpata wa bahati yako, hata uwe maskini unaweza kung’ara na maisha yako yakatawaliwa na faraja, ila ukitumbukia sehemu ambayo si yako, ni mateso ya moyo na sononeko lisilokwisha.
Hapa nifafanue kuwa yule ambaye anajiona yupo kwenye uhusiano salama, basi aendelee hapohapo kwa sababu ndipo kwenye bahati yake. Kwa wale wenye maumivu pale walipo, basi wajiangalie mara mbilimbili. Maisha yanaendelea. Maisha bora yanajengwa na mtu mwenye akili iliyotulia.
Huwezi kuwa na matatizo, akili haitulii kwa sababu ya misukosuko ya kimapenzi, ukadhani kwamba utajenga maisha imara. Hapo utakuwa unajidanganya. Tibu kwanza janga lako la mapenzi ili maisha yako yanyooke. Ikiwezekana, jipe muda wa kukaa ‘singo’. Inawezekana.
Beba zingatio kuwa lipo kundi la watu wanaowachezea wenzi wao lakini maisha yao ya kimapenzi bado ni imara. Japo anayetendwa ni maumivu kwake, ila mtendaji ni sawa tu. Haumii, anamnyanyapaa mwenzi wake na anaendelea kupendwa. Ni bahati tu.
Wewe unasaga miguu na kuumiza kichwa. Kila siku unajitahidi kumtafuta mwenzi bora wa maisha yako lakini hujampata. Badala ya furaha, unavuna machungu mtindo mmoja. Usijione una bahati mbaya, badala yake endelea kuitazama mbele kwa matumaini.
Huyo huelewani naye kwa sababu siyo wa bahati yako. Wako yupo na bahati mbaya hujamfikia. Jambo la kufanya si papara, kuwa mtulivu, utampata kwa urahisi. Ukijifanya bingwa wa kuwapanga na kuwapangua, hutafanikiwa, matokeo yake utampita na mwenzi bora wa maisha yako bila kujua.
Penda kutazama mifano kwa walio karibu yako. Je, wanaishi vipi na wenzi wao? Kama nao picha haziendi, tambua kwamba wanalazimishana. Watu wanaopendana, haiwezekani kila siku wakawa wanasumbuliwa na migogoro. Kuna mawili, moja litakuwa sahihi.
Mosi; wote hawapendani ila walijikuta wapo pamoja kwa mvuto wa tamaa za mwili, nao wakajidanganya ni mapenzi, hivyo wakawa pamoja. Pili; kama mosi haikuwa sahihi, basi itakuwa mmoja anapenda, mwingine analeta utani, hivyo kufanya misuguano isiyoisha.
Mapenzi yana nguvu yenye mvutano mithili ya sumaku. Hoja hapa ni kuwa endapo kutakuwa na mapenzi ya kweli, mara nyingi mtajikuta mpo kwenye mstari mmoja, kwani kuna nguvu ya asili ambayo hamuioni, inayowaweka pamoja muda wote. Ni nadra kutofautiana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment