Usithubutu ‘kufeki’, penzi bora hujitengeneza lenyewe Part -2.


Usithubutu ‘kufeki’, penzi bora hujitengeneza lenyewe Part -2.


Bila shaka wasomaji wangu wote ni wazima wa afya na mnaendelea na majukumu yenu. Tunaendelea na mada yetu kuanzia pale tulipoishia.
Twende pamoja...
MZEE Nelson Mandela ‘Madiba’, alitoa talaka kwa bibi yetu, Winnie. Waliishi miaka mingi, wakazaa watoto ambao wengine kwa sasa ni wakubwa kabisa. Baadaye akagundua Winnie si bahati yake, leo yupo kwenye ndoa na Graca Machel, maisha yanaendelea.
Kumbe Graca ndiye bahati ya Mzee Mandela. Ilivyo ni kwamba Winnie alitangulia kwa lengo la kukamilisha safari ya maisha ya babu yetu huyo anayeheshimiwa mno duniani. Chukua mfano huo, halafu jipe matumaini. Maisha ni matamu mno bila ya huyo wako ambaye si bahati yako.
Napenda tena nitie mkazo kwamba mapenzi ni magumu. Kama Mandela yalimuumiza, inashindikana vipi kwako? Ukimpata wa bahati yako, hata uwe maskini unaweza kung’ara na maisha yako yakatawaliwa na faraja, ila ukitumbukia sehemu ambayo si yako, ni mateso ya moyo na sononeko lisilokwisha.
Hapa nifafanue kuwa yule ambaye anajiona yupo kwenye uhusiano salama, basi aendelee hapohapo kwa sababu ndipo kwenye bahati yake. Kwa wale wenye maumivu pale walipo, basi wajiangalie mara mbilimbili. Maisha yanaendelea. Maisha bora yanajengwa na mtu mwenye akili iliyotulia.
Huwezi kuwa na matatizo, akili haitulii kwa sababu ya misukosuko ya kimapenzi, ukadhani kwamba utajenga maisha imara. Hapo utakuwa unajidanganya. Tibu kwanza janga lako la mapenzi ili maisha yako yanyooke. Ikiwezekana, jipe muda wa kukaa ‘singo’. Inawezekana.
Beba zingatio kuwa lipo kundi la watu wanaowachezea wenzi wao lakini maisha yao ya kimapenzi bado ni imara. Japo anayetendwa ni maumivu kwake, ila mtendaji ni sawa tu. Haumii, anamnyanyapaa mwenzi wake na anaendelea kupendwa. Ni bahati tu.
Wewe unasaga miguu na kuumiza kichwa. Kila siku unajitahidi kumtafuta mwenzi bora wa maisha yako lakini hujampata. Badala ya furaha, unavuna machungu mtindo mmoja. Usijione una bahati mbaya, badala yake endelea kuitazama mbele kwa matumaini.
Huyo huelewani naye kwa sababu siyo wa bahati yako. Wako yupo na bahati mbaya hujamfikia. Jambo la kufanya si papara, kuwa mtulivu, utampata kwa urahisi. Ukijifanya bingwa wa kuwapanga na kuwapangua, hutafanikiwa, matokeo yake utampita na mwenzi bora wa maisha yako bila kujua.
Penda kutazama mifano kwa walio karibu yako. Je, wanaishi vipi na wenzi wao? Kama nao picha haziendi, tambua kwamba wanalazimishana. Watu wanaopendana, haiwezekani kila siku wakawa wanasumbuliwa na migogoro. Kuna mawili, moja litakuwa sahihi.
Mosi; wote hawapendani ila walijikuta wapo pamoja kwa mvuto wa tamaa za mwili, nao wakajidanganya ni mapenzi, hivyo wakawa pamoja. Pili; kama mosi haikuwa sahihi, basi itakuwa mmoja anapenda, mwingine analeta utani, hivyo kufanya misuguano isiyoisha.
Mapenzi yana nguvu yenye mvutano mithili ya sumaku. Hoja hapa ni kuwa endapo kutakuwa na mapenzi ya kweli, mara nyingi mtajikuta mpo kwenye mstari mmoja, kwani kuna nguvu ya asili ambayo hamuioni, inayowaweka pamoja muda wote. Ni nadra kutofautiana.,,itaendelea........
Usithubutu ‘kufeki’, penzi bora hujitengeneza lenyewe..t...PART.1

YALIANZA kuumbwa maisha halafu mapenzi ndiyo yakafuata. Aliumbwa Adam, baadaye akaletewa Hawa kisha mapenzi ndiyo yakaanza. Hii ina maana kuwa maisha yalianza kwa upande wa Adam kabla ya mapenzi. Hili zingatia katika kutafsiri sura ya kule uendako maishani.
Hata wewe jiulize, ulipozaliwa ulikuwa hujui mapenzi ni nini? Hapa sizungumzii mapenzi ya kawaida, yale ambayo mtu anaweza kuyapata kutoka kwa wazazi wake au ndugu zake wengine. Yanayotajwa hapa ni mapenzi katika maana yake halisi. Mapenzi ya ndani kabisa.
Yale ambayo huwafanya watu waziache familia zao za asili na kwenda kutengeneza nyingine. Nayazungumzia yale ambayo yanawafanya watu wanauana, wengine wanakunywa sumu. Yanayowatesa watu mpaka wanashindwa kula na kadhalika.
Swali ni moja; Kama iliwezekana kuishi bila mapenzi mpaka ulipofikisha umri wa utu uzima, iweje leo yakutawale mpaka ushindwe kujiendesha mwenyewe? Haipingiki kwamba mapenzi ni muhimu lakini hayapaswi kutawala ubongo wako. Utafeli haraka.
Mapenzi ni mazuri kwako endapo utaweza kuyamudu. Yakikushinda wewe ni mtumwa. Kaa, tuliza akili halafu tafakari. Baada ya hapo chukua hatua. Haijalishi umeshaathirika kiasi gani, muhimu kwako ni kuzingatia kwamba inawezekana kubadilika.
Japo unapenda mno, unajitahidi kuonesha unajali katika mazingira yoyote. Umemfanya mwenzako sawa na mboni yako kwa namna unavyomtunza. Kama yeye harudishi mapenzi unayompa, hajali na kukupa heshima kulingana na ile unayompa, angalia maisha yako kwanza.
Angalizo; Ukimng’ang’ania sana, atakugeuza punda. Atajipa kiburi kwamba anaweza kufanya lolote nawe utatii kwa sababu unampenda. Usidanganywe na imani zisizokuwepo, binadamu hawekwi kiganjani wala kwenye chupa. Una akili hai, tazama mbele pengine hapo si kwenye bahati yako.
Kama anashindwa kukuthamini kwa namna unavyompenda, hawezi kuyapenda maisha yako. Atakutumia atakavyo, akishatimiza malengo yake, atakuacha ukihangaika na dunia. Wakati huo yeye yupo na mtu wake anayempenda, atakuwa anakucheka.
Akikaa na marafiki zake, atawaambia kwamba yeye ndiye alikuwa nyota yako, kwamba ulipokuwa naye maisha yako yalikuwa rahisi na hivi sasa umechoka baada ya kuachana naye. Hatazungumza jinsi alivyokutesa, akakuweka roho juu, akakusababishia maumivu ya moyo mpaka ukashindwa kutekeleza majukumu yako.
Usikubali muda wako upotee bure. Maisha yako ni ya thamani, yupo nawe leo lakini kesho inawezekana si wa kwako. Lakini maisha yatabaki kuwa yako kwa mazingira yoyote yale. Hoja yangu hapa ni kwamba mapenzi yasikutawale mpaka ukasahau maisha.
Wengi waliishia njiani, walijiaminisha wanapendana kutoka ndani ya kuta za nyoyo zao. Wakaahidiana kuwa hakuna kitakachowatenganisha. Siku yalipotimia, ahadi zote zikayeyuka. Hupaswi kung’ang’ania ulipo, bali yafaa ujiulize, je, hapo ndipo kwenye bahati yako?
Watu kwenye ndoa wameachana, si kwamba walipenda la hasha! Wachumba wanaishia njiani, vilevile marafiki walioamini wanachanua, wakapeana mkono wa kwa heri. Ni vizuri kukubali kwamba jitihada hazishindi kudura. Pamoja na mapenzi yako makubwa, unavyojali, unavyomheshimu kama si bahati yako hamuwezi kudumu.
Haijalishi utu wako ni wa thamani kiasi gani.
NI KOSA KUMWAMBIA MPENZI WAKO MUWAPO FARAGHA KUWA ''UMECHOKA''........PART .1.

TUNAENDELEA kuyajadili mapenzi. Kuna vitu vingi ambavyo vinasababisha uhusiano wa wengi kudumu. Maelewano, kusikilizana, kuheshimiana na mengineyo, lakini unyumba ni chachandu yenye nguvu. Nimekuwa nikiwashauri wasomaji wangu vitu vingi lakini hili nimeteua nilichambue kwa ufafanuzi leo.
Kuna watu ambao wamekuwa hodari kujisifu kuwa wao hutoa unyumba kwa ‘kibaba’. Yaani huwapimia wenzi wao. Kwa mitazamo yao, hujiona wapo sahihi. Tabia hii ipo kwa wanawake zaidi, japo kuna wanaume ambao nao ni wagumu kutekeleza mahitaji ya wapenzi wao.
Hata hivyo, kuna kitu cha kuweka sawa hapa; Wakati mwanamke anapobana ‘staftahi’ kwa mwenzake, huhesabika ni mchoyo! Kwa mwanaume yeye huonekana ni goigoi. Kwamba mambo hayawezi ndiyo maana hatekelezi shughuli. Ataambiwa ana tatizo la zile nguvu zetu!
Mwanamke anaweza kujisifu hata kwa wenzake. Akiwa kwenye vikao vya kusukana au katika soga nyingine, atajimwagia sifa tele kwamba yeye inaweza kupita miezi bila kuingia uwanjani na mwenzi wake. Hili, linawafanya wanaume wengi wateseke na matokeo yake hutafuta tiba mbadala.
Mwanaume hawezi kujisifu kwa marafiki zake kuwa yeye huwa akisumbuliwa na mwenzi wake, humpa mgongo! Ni wazi akisema hivyo atachekwa. Yaani mwanamke kugomea kutoa unyumba ni ushujaa wakati mwanaume akikataa, atachukuliwa kwamba ana tatizo la kiafya! Dhana hii sikubaliani nayo, kwahiyo nahitaji kutoa shule!
Kwangu mimi, kila aliye mvivu wa kuingia shughulini ana tatizo! Kwa mwanaume na mwanamke, wote wana kasoro ya nguvu, kwa maana hiyo wanahitaji tiba mbadala ili waweze kusherehekea tendo. Wanatakiwa kuboresha mvuto wao katika ndoa au uhusiano, na nafasi ya kutekeleza hilo ipo!
Ni lazima watu waheshimu uhusiano wao wa kimapenzi. Pia waelewe kwamba moja kati ya vitu vinavyoshikilia penzi lao ni unyumba. Ni wakati muafaka kwako sasa, kuachana na mawazo ya kale. Punguza uvivu na ujue kuwajibika inavyotakiwa, kwa maana ni njia ya kutibu amani yako mwenyewe na mwenzio.
Utafiti unaonesha kwamba asilimia kubwa ya ndoa zinazovurugika kila siku, nyuma yake huwa na shambulio la wanandoa kutopeana huduma ya tendo. Kwamba, wanavumiliana lakini mwisho sauti itasikika kwa majirani. Watakapokuwa wanagombezana usiku, siri hugeuka sirini.
Tendo la ndoa, hukamilisha furaha ya wawili walioamua kupendana. Tunapoamua kuacha siasa na kuzingatia ukweli kwa vipimo vyake, watu wengi (hasa wanaume), wanapoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, lengo lao la kwanza ni kutimiza haja zao kimwili kwa mtu husika. Nazungumza kwa utafiti!
Walikutana barabarani, akavutiwa ndiyo maana akaanza misele. Anapofanikiwa, vikwazo vya baadaye, inakuwa siyo matarajio yake. Alichotarajia ni kwamba baada ya kukubaliana kuingia kwenye sehemu yenu ‘spesho’, atakuwa hapimiwi! Kwa kiwango chochote atakachohitaji, mwenzi wake atamridhia.
Aghalabu, wapenzi ambao wanajikuta wapo kwenye mgogoro wa tendo, mara nyingi hukabiliwa na tatizo la usaliti. Ni theluthi moja ya wanawake wanaoweza kumvumilia mwanaume ambaye hamtoshelezi kimwili, wakati kwa wanaume ni moja ya kumi tu ndiyo wenye kuvuta subira mpaka siku watakapokumbukwa.
“Huyu mbona yupo hivi, kila siku anasema kachoka, atakuwa na mtu huko nje,” ni kauli ambayo ni rahisi kupita kichwani kwa mwanamke, pale ambapo anakabiliana na mwenzi ambaye haguswi chochote na tamaa za mwili, ingawa inaelezwa kwamba ni moja ya kumi ya wanawake ndiyo hukosa usingizi kwa kunyimwa tendo.itaendelea......

No comments:

Post a Comment