Watu wenye tabia hii husababisha mapenzi kuwa magumu-3


Na:Luqman Maloto
Bila shaka msomaji upo safi na unaendelea na majukumu ya ujenzi wa taifa. Tunaendelea na mada yetu kuanzia pale tulipoishia wiki iliyopita. Twende pamoja...
Kundi hilo ndilo linatajwa kwamba wahusika wake hawajatulia.
Hata hivyo, upo ukweli uliotimia kuwa mitaani kwa jamii ya watu wa kawaida, wapo wachafu kuliko. Mwanamke mmoja anaweza kuwapanga wanaume watano kwa siku. Akitoka huyu anakwenda kwa mwingine. Anabadili nyumba za kulala wageni.
Huyu, hajitambulishi kama changudoa. Atasimama pembeni na kwamba yeye ni mtu mwenye heshima zake. Akiwaona machangudoa usiku wa manane wakiwa wamejipanga mawindoni na mavazi yao ya nusu uchi, atawalaani. Ni msemo wa nyani haoni makalioni kwake!
Huko nyuma nilishawahi kueleza mfano wa wanandoa kusalitiana. Nikabainisha kwamba baadhi ya wanaume hufanya makosa pale wanapowakataza wanawake wao kufanya kazi. Eti wanataka wakae tu nyumbani. Hapa ndiyo kuna jambo, kwani mtu anapokaa bila kazi, hukaribisha hisia za karibu.
Hii ikanifanya nijenge hoja kutokana na muongozo wa kisaikolojia kwamba akina mama wa nyumbani, ni kundi hatari mno kusaliti ndoa. Mara nyingi wanakuwa hawapo bize, kwa hiyo hisia za kimapenzi zinakuwa karibu na matokeo yake hujikuta wakifanya zinaa na watu wa kushangaza.
Hujawahi kusikia mke wa mtu katembea na ‘houseboy’ wake? Vipi mwanamke kufanya zinaa na mdogo wa mume wake? Je, muuza bucha kujilia vyake nyakati za mchana kwa ofa za robo ya nyama anayomuongezea mke wa mtu aliyekwenda kununua kilo mbili? Hayo yapo kwenye mazingira yetu ya kila siku.
Kila siku wauza magenge na maduka, wanaingilia ndoa za watu. Nafasi hizo wanazipata kwa sababu ya kutokuwepo ubize kwa wanawake hao. Asili yetu tunapenda utani, hivyo wakitaniana mara mbili, mwanamke anahama kihisia. Keshokutwa asubuhi mume akiondoka, huyo anakimbilia gengeni.
Huu ni mfano katikati ya mada yetu. Mtu wa aina hii akiwaona machangudoa barabarani, atawalaani kupita kiasi. Hata hivyo, mtindo wa maisha yake hauna tofauti na changudoa kutokana na ukweli kwamba mtu mwenye staha na heshima, hawezi kujilimbikizia vidumu. Mume usiku, mchana muuza bucha au houseboy, haijakaa vizuri.
Inabidi kutoa mfano wa aina hii kutokana na ukweli kwamba masistaduu wanaweza kukaa vibarazani na kusogoa kuwa mbona wake za watu wanaojionesha ni watu makini, nao wanacheza sana mechi za nje?

No comments:

Post a Comment